- Kuzungumzia mafanikio ya Parokia ya Utatu Mtakatifu Changanyikeni kwa sasa inaweza ikaonekana ni mapema sana, pengine ingekuwa mwafaka kwa wajukuu zetu wakati huo watakuwa na mengi ya kusema, lakini ni wajibu kukiri kwamba yote yaliyomo, mfano majengo, idadi ya wakristo inayoongezeka yanaweza kufananishwa na ile mbegu ya haradali inayozungumziwa kwenye Biblia ambayo imebahatika kuangukia kwenye udongo wenye rutuba na baadaye ikaanza kumea na kuzaa matunda (Mk 4:30-32).
- Kwa wale wakristu wa kwanza walioasisi ujenzi wa kigango cha Changanyikeni pale ushirika na baadaye kupata eneo hapa tulipo hawakufahamu kwa dhati kama ndoto hii ingetimia mapema hivi yaani kuwa na huduma za misa kila siku wakati wao walikuwa wanahudumiwa na parokia ya Chuo Kikuu na Mt.Paulo Msewe.
- Ikiwa kigango cha Mt. Petro Changanyikeni iliadhimisha pia misa takatifu ya komunyo ya kwanza ambapo watoto wetu kwa mara ya kwanza walipata sakramenti ya ekaristi takatifu, Aidha sakramenti zingine zimewahi kutolewa hapa ikiwa kama kigango mfano misa ya ndoa takatifu. Na tarehe 14 Oktoba 2017, kwa mara ya kwanza Parokia ya Utatu Mtakatifu imeadhimisha Misa Takatifu kwa ajili ya sakramenti ya Ubatizo wa watoto wachanga.
- Lingine ambalo ni sehemu ya mafanikio ni kuadhimisha sikukuu ya ekaristi takatifu kwa maandamano na kabla haijawa parokia tulikuwa tukiadhimisha sherehe ya somo wa Kigango chetu Mt. Petro Changanyikeni kila tarehe 29 Juni, kutokana na msingi huo tutaendelea kuadhimisha sherehe ya somo wetu wa Parokia yaani Utatu Mtakatifu kama ilivyopangwa katika liturjia ya Kanisa Katoliki.
- Paroko wetu Padre Gallen Mvungi, tangu afike Parokia ya Utatu Mtakatifu amefanikiwa kuimarisha na kupanua wigo wa huduma za kiroho kwa kuandaa taratibu mbalimbali ikiwemo kuzitembelea Jumuiya zote na hivi karibuni atakamilisha kuzitembelea kaya mmoja mmoja na kujadilaiano nao changamoto mbalimbali za kiroho na pia wakti alipozitembelea jumuiya zote, aliadhimisha ibada ya misa takatifu, kuwafafanuliwa masuala mbalimbali ili kukuza uinjilishaji kwa wanaparokia ya Utatu Mtakatifu. Aidha kila ijumaa huwatembelea waumini wagonjwa kuwashauri, kuwapa huduma za kiroho kupitia sakramenti ya kitubio na ekaristi takatifu na mpako mtakatifu kwa walio katika hatari ya kufa, nk.
- Parokia ya Utatu Mtakatifu, tangu ikiwa ngazi ya kigango imekuwa mstari wa mbele katika kushiriki kwenye masuala mbalimbali ya kukuza Imani yao, mfano hija kiparokia, kidekania, na hata kijimbo. Pia kushiriki kikamilifu katika semina mbalimbali za kiroho zilizokuwa zikitolewa kwa weledi mkubwa na Monsinyori Mbiku hasa katika vipindi vikuu vya mwaka wa kanisa, yaani Kabla ya Krismasi na kabla ya Pasaka, ili kuwaandaa wahamasishaji wa shughuli za kiroho na ujenzi wa kanisa Changanyikeni na kituo cha watoto cha Parokia ya Chuo Kikuu ambapo waumini wa Changanyikeni ni washiriki wakuu, dhana ya uongozi katika kanisa na sifa zinazotakiwa.
- Wanaparokia ya Utatu Mtakatifu wameshiriki katika matendo ya huruma vipindi vya pasaka kwa ajili ya wahitaji, kama vile wafungwa, wazee, watoto yatima na wengine wenye matatizo mbalimbali na maskini wote katika maeneo yetu na nje ya Changanyikeni kadiri ya mwongozo wa msimamizi wa Kigango, Paroko wa Parokia ya Chuo Kikuu.
- Kushiriki katika uzinduzi na utekelezaji wa kauli mbiu zote za mwaka wa Kanisa, mfano Msalaba Mtakatifu, Mwaka wa Imani, Mwaka wa Familia, Mwaka wa Huruma ya Mungu na sasa Mwaka wa Mapadre.